Dar es salaam, Tanzania
Kuna haja ya wasomi bungeni?
Katika dunia ya leo ambapo majukumu ya kibunge yanahusisha takwimu, sheria na diplomasia, ni rahisi kujenga hoja kuwa wabunge wanapaswa kuwa na vyeti vya elimu ya juu. Kwani vyeti hivyo ni viashiria vya nidhamu; mahudhurio, utii, kumaliza kazi kwa wakati, kufundishika, taaluma fulani, uwezo wa kutathmini na kwa nchi zenye kuoanisha itikadi na elimu; itikadi na mengineyo.
Kama inanilazimu nitaje kimoja tu, basi ingekua ujuzi wa kufanya tathmini bila ya kujali taaluma, kwani hakuna mtaalam wa kila kitu.
Dhana ya “mbunge bora ni mbunge msomi”
Bila shaka ni sifa njema mbunge kuwa amehitimu chuo kikuu, kuwa mwenye uwezo wa kuelewa uchumi, sheria, na weledi katika hoja za kisera. Ni kweli, elimu huongezea viongozi ufanisi wa kuzitabiri kesho kwa kutumia jana, kusoma bajeti na kuelewa mikataba.
Bunge ni kioo cha umma au chuo?
Katika taifa la kidemokrasia wagombea wanapaswa kujinadi. Kuwaambia wapiga kura kwanini wanatosha zaidi kuwa-wakilisha dhidi ya wengine.
Kuchuja wagombea kwa kigezo cha usomi pekee kinazua tafakuri:
-Wapiga kura hawataki wasomi?
Mpiga kura wa kawaida huishi athari za sera kila siku, bei ya unga, huduma za afya, au usalama. Anaweza kutambua kwa hisia na uzoefu halisi nani anamjali na nani ni mbinafsi.
Tukumbushane makubaliano:
🇹🇿 Tanzania – Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (Marekebisho ya 2020)
Ibara ya 66(1):
“Bunge litakuwa na Wabunge watakaopatikana kwa kuchaguliwa na wananchi...”
(“Parliament shall consist of Members elected by the people…”)
Niwapatie nukuu ya kauli ya aliekua mbunge wa Tanzania bila kutaja jina ama chanzo,
“Wewe utanionya nini kwa mfano, wewe darasa la saba, mimi hapa, daktari wa falsafa, mwalimu wa vyuo vikuu mbalimbali utanionya nini?”
Pengine lakini pengine
Pengine jawabu la maendeleo kijamii sio bunge la wasomi bali jamii ya wasomi, kwani jamii ya namna hiyo haitakubali kuwakilishwa na wale ambao hawaiakisi jamii yao.
Pengine kiongozi bora ni yule anayetokana na umma, alietumwa na umma, anaewakilisha umma.
Pengine umma unataka ujue mwakilishi wao ameishi kero zao.
Pengine umma unataka mwakilishi anaetatua changamoto zinazowakabili kwasababu ni za kwake pia, na si kwasababu wamebahatika kuletewa msomi.
Pengine kuwalazimishia wapiga kura wagombea kwa msingi wa usomi ni kutokua na imani kwa utashi wa umma.
Pengine taasisi ya kiuwakilishi itapata ushauri kutoka taasisi ya kitaaluma utakapohitajika, kwani bunge haliwezi tosha mtaalam wa kila fani na jamii ina shida kutoka kila fani.
Pengine wanataaluma wawakilishwe na jumuiya za kitaaluma.
Pengine lakini, pengine.