YALIYOMO
Loading titles...

"Ukweli" na ukweli, mapacha wa wazazi tofauti.

Tanzania, Dar es salaam.

Daima binadamu tumekua tukijimilikisha ukweli. Kwa maslahi binafsi ama matabaka tuliyomo.

Kwenye ulimwengu wa kidigitali, ambapo dole gumba ni alama ya kiushawishi wa nini ni "kweli", mapambano ya kumiliki "ukweli" yamepamba moto.

Teknolojia ya intaneti imekuja na ahadi ya kutoa "ukweli" mikononi mwa wachache kwa kusogeza macho na masikio ya umma kwa kila aliye tayari kusimulia. Hivyo, nguvu za wamiliki wa "ukweli" zimefifishwa.

Hata hivyo, uhuru huu hauji bila changamoto; kadri sauti zinavyoongezeka, ndivyo inavyokuwa vigumu kutofautisha ukweli na "ukweli"..

Historia ya "ukweli" kama simulizi la madaraka

Historia imejaa matukio ambapo “ukweli” ulikuwa kile tu ambacho mamlaka inakitamka. Maandiko tofauti-tofauti yanatoa simulizi za watu; matabaka fulani, kuwa “waliopendwa,” “walioteuliwa,” au “waliobarikiwa” zaidi.

Wafalme walidai haki ya kifalme, kiutawala wamepewa na Mungu. Watawala wa kikoloni walihadithia;wanahdithia historia inayodogosha madhila ya uvamizi. Madikteta hutengeneza simulizi zinazowatukuza wao na kufuta uwapo wa wapinzani.

Katika mazingira kama haya, "ukweli" ni simulizi la yeyote anayehadithia. Msimulizi ndiye anaeamua nini umma unaamini. Hivyo basi, "ukweli" ni bidhaa: unanunuliwa, unauzwa, au kunyang’anywa.

Falsafa kuhusu umiliki wa "ukweli"

Falsafa kutoka enzi za Socrates hadi Hannah Arendt zimetoa hoja kuwa ukweli haupaswi kumilikiwa na mtu yeyote; unapaswa tu kuwepo.

Hakuna taasisi, serikali, au jukwaa la "ukweli" bila ridhaa yako. Kila mmoja wetu ni mdau, na hatimiliki ya umiliki wa "ukweli" hutolewa na wewe unaehadithiwa, haswa unaposhindwa kuhoji dhana ulizonazo, kuhoji "ukweli" uliozoea. Unapoamua kujidhulumu kwa kuruhusu mwingine afikiri kwa niaba yako. 

Pengine suluhisho ni kukubali kubaki Edeni kwa kukumbatia ujinga kwani upo usalama katika ujinga? Na hakuna uerevu katika "ukweli" wa nyoka; hakuna usalama katika kujua jema na baya?

Tunawezaje kujilinda dhidi ya "ukweli"?

Pengine tunaweza kujilinda dhidi ya "ukweli" kwa:

  • Kutambua kile tunachotaka kusikia, 

  • Kutompatia mtu au taasisi mamlaka ya "ukweli",

  • Kusikiliza “kelele, upuuzi, usumbufu” za "uliowazidi maarifa, busara, hekima na hadhi", tofauti na "ukweli"  kama unavyoujua; kama unvyokupa ukubwa.

Pengine ukweli si maneno na matendo tu, bali huamuliwa na muktadha; na pale muktadha unapobadilika, unazaliwa "ukweli" mpya.

Pengine ukweli, hauna mwenye hati miliki.

Pengine kodi tunayopaswa kulipia kuishi katika ukweli ni udadisi na unyenyekevu wa kukubali kuwa wajinga ndo waliwao na wewe uko katika menu.